PHOTO:COURTESY
Rais Uhuru Kenyatta ametoa makataa ya
siku 5 kwa viongozi wa kaunti ya Marsabit kuhakikisha kwamba wanapata suluhu ya
kudumu kwa machafuko na vita vya kikabila ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa katika
kaunti hiyo la sivyo hatua kali zichukuliwe.
Kwenye mkutano uliandaliwa katika ikulu
ya rais Jijini Nairobi, gavana wa kaunti ya marsabit Mohamud Ali alitwikwa
jukumu la kuwaleta pamoja viongozi wenzake jimboni humo ili kuhakikisha kuwa
wanapata suluhu ya shida hiyo katika muda huo mfupi.
Kiongozi wa taifa aliyeghadhabishwa na
machafuko ya mara kwa mara marsabit alitoa fursa ya mwisho kwa viongozi hao
kuhakikisha kwamba wanapata suluhu ya changamoto hizo la sivyo mwenyewe
atachukua hatua kali.
Hata hivyo katika ujumbe wake kwa
viongozi hao, rais Uhuru Kenyatta aliwataka kutambua mbinu za kutatua shida
hiyo kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa, na kuwataka wasilaumu serikali iwapo
hatua hiyo itaafikiwa.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wabunge wa kaunti
hiyo ya marsabit, viongozi wa kidini, uongozi wa bunge la kaunti ya Marsabit na
maafisa wa usalama.
Waziri wa masuala ya ndani Daktari Fred
Matiangi, kamishna wa ukanda wa mashariki mwa Kenya, Isiah Nakoru, na kamishana
wa kaunti ya marsabit Paul Rotich ni miongoni tu mwa maafisa wa usalama
waliohudhuria mkutano huo.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria
mkutano huo ni pamoja na gavana Mohamud Ali, wabunge Dido Ali Rasso wa Saku,
Francis Chachu Ganya wa North Horr, Musa Arbelle wa Laisamis na Qalicha Gufu wa
Moyale, seneta Naomi Jillo Waqo , mwakilishi wa kike Safia sheikh Adan na spika
wa bunge la kaunti ya Marsabit, Mathew Loltome na kiongozi wa wengi katika
bunge hilo, Alkano Konso.
Hata hivyo waziri wa fedha, Ukur Yatani
hakuhudhuria mkutano huo kwani aliarifiwa kuwa nje ya nchi kwa shughuli rasmi
za kikazi.
Viongozi wa dini waliohudhuria ni pamoja
na Askofu wa kanisa katholiki jimbo la Marsabit, Peter Kihara, Sheikh Mohammed
Noor Kuli, miongoni tu mwa viongozi wengine.
Wakati hayo yakijiri, mbunge wa
Laisamis Musa Arbelle amehoji kuwa wao kama viongozi hawana budi ila kuafikia
makataa ya siku tano waliopewa na rais Uhuru Kenyatta kutafuta suluhu ya shida
inayokumba gatuzi hili.
Arbelle amesema kwamba kiongozi wa
taifa alitaka kujua changamoto inayopelekea vita vya mara kwa mara jimboni na
kuonya kwamba iwapo viongozi watafeli kuleta suluhu ya shida zinazokumba kaunti
hiyo hatua kali zitachukuliwa.
Kutokana na mkataa ya siku tano,
viongozi wa kaunti hiyo wameafikiana kufanya kikao na kuanza majadiliano ya
kutafuta suluhu ya shida ya kaunti hiyo kuanzia Jumatatu wiki ijayo katika taasisi ya
Kenya school of government, jijini Nairobi.
Kulingana na mbunge huyo, waziri wa
masuala ya ndani, Fred Matiangi amehoji kwamba sasa rais Uhuru Kenyatta ndiye
amechukua jukumu la kuhakikisha kwamba shida hiyo inasuluhishwa.
Viongozi hao pia wametakiwa
kutolaumiana na badala yake kuketi pamoja na kutafuta suluhu ya shida ya
Marsabit huku Wakaazi wa kaunti hiyo pia wakitakiwa kujihusisha katika juhudi
za kuleta amani ya kudumu.